Jumanne, 17 Septemba 2019

SABABU ZA WANAWAKE KUTOKWA NA UCHAFU SEHEMU ZA SIRI

Kuna tatizo linalowasumbua wanawake wengi hapa nchini na duniani kwa ujumla, hilo ni tatizo la kutokwa na uchafu unaotoa harufu mbaya sehemu za siri.  Kitaalamu hali ya mwanamke kutokwa na majimaji hayo ambayo kitaalamu huitwa vaginal fluids, yenye rangi nyeupe au ya njano. Wakati mwingine hali hiyo huwa ya kawaida na wala siyo tatizo hasa kama majimaji hayo siyo mazito sana na wala hayatoi harufu kali.
Lakini endapo majimaji yanayotoka yapo katika hali ya ute mzito wenye rangi nyeupe au kahawia, yanatoa harufu kali na yanawasha, basi hiyo ni ishara ya ugonjwa uitwao Vaginosis. Majimaji au ute unaoteleza kutoka sehemu za siri huwa ni njia inayowezesha viungo vya uzazi vya mwanamke kujisafisha na kuutoa uchafu wa seli zilizokufa na mabaki ya damu ya hedhi nje ya mwili.
Pia huvikinga viungo vya uzazi dhidi ya maambukizi ya bakteria au fangasi wanaosababisha magonjwa.Kwa kawaida majimaji hayo huwa hayatoi harufu na huwa na rangi nyeupe au ya njano lakini yakitoa harufu, huwa ni ishara ya tatizo. Majimaji hayo huwa na asidi ya Lactic ambayo huzuia kuzaliana kwa vijidudu vya maradhi na huzalishwa kwenye tezi za Bartholin (Bartholin’s glands) zilizopo kwenye shingo ya mlango wa uzazi (Cervix).
Kwa kawaida, mwanamke hutoa kiasi cha gramu mbili za seli zilizokufa kutoka kwenye mji wa uzazi na gramu tatu za ute mwepesi kila siku. Kiwango hiki huweza kuongezeka au kupungua kutegemeana na mzunguko wa siku za mwanamke yaani hedhi.
Kuna wakati ute huwa mwepesi na unaovutika mfano wa ute wa yai la kuku na kuna wakati huwa mzito kiasi na wenye rangi ya njano. Ute huu ni wa kawaida na huwatoka wanawake wote hususan baada ya kuvunja ungo.


SABABU ZA KUTOKWA NA UCHAFU NA HARUFU MBAYA
Kuna sababu nyingi ambazo husababisha mwanamke kutoa ute au majimaji yasiyo ya kawaida kutoka kwenye sehemu zake za siri. Sababu kubwa ni maambukizi ya bakteria wanaosababisha magonjwa kama Trichomoniasis, Candidiasis, Gonorhear au uambukizo wa bakteria Candida albicans, Vaginosis Bakteria n.k husababisha mwanamke kutokwa na uchafu unaoambatana na harufu kali.
Pia mabaki ya vitambaa, tishu au pedi ambazo hazikutolewa wakati wa hedhi huweza kusababisha tatizo hili. Usafi wa sehemu za siri usipozingatiwa hususan mwanamke anapokuwa kwenye siku zake za hedhi, huweza kuwa makazi mazuri ya bakteria wanaosababisha harufu hiyo kali.
DALILI ZA UGONJWA
Mwanamke mwenye tatizo la Vaginosis huwa na dalili kubwa ya kutokwa na ute na majimaji yasiyo ya kawaida (uchafu) kutoka sehemu za siri. Uchafu huu huwa unatoa harufu kali kama shombo ya samaki au kitu kilichooza na huambatana na maumivu makali ya tumbo chini ya kitovu.
Wakati mwingine uchafu wenye rangi kama ya kijani hutoka, kuwashwa na kuchomachoma sehemu za siri, mgonjwa asipopatiwa tiba haraka husababisha vidonda sehemu za siri. Mwanamke anapoona anatokwa na ute uliochanganyikana na damu hata kama hayupo kwenye siku zake, hii ni dalili nyingine ya Vaginosis au akisikia maumivu makali wakati wa tendo la ndoa pia ni dalili za ugonjwa huu.

MATIBABU NA USHAURI
Tatizo hili hutibika hospitalini baada ya vipimo vya kitaalamu kuchukuliwa na daktari mtaalamu mwenye uzoefu wa kutosha juu ya magonjwa ya wanawake. Dawa za kupaka na za kumeza za vidonge huweza kumaliza tatizo hili. Ni makosa kutumia dawa bila kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa daktari mtaalamu wa afya kwa sababu dawa ni sumu isipotumika vizuri.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni