Ijumaa, 7 Februari 2020

UMUHIMU WA WATOTO KULALA MCHANA


Wazazi wengi huwalazimisha watoto kulala mchana bila kujua umuhim wa kufanya ivo, wengine hawajui na wala hawafanyi jitihada za kuwalaza watoto mchana. Wengine hufanya ivo kupunguza vurugu na mikimiki ya watoto, Wengine wanafanya kwa sababu ya mazoea, kuiga kwa majirani na sababu nyingi zingine. Tambua umuhim wa mtoto kulala mchana;
  • Husaidia ukuaji wa mtoto hasa wa ubongo na viungo vya mwili
  • Inaongeza ubunifu na ufanisi katika shule na maeneo mengine
  • Inaongeza uwezo wa kujifunza na kumbukumbu
  • Inapunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo
Kwa sababu izo ni muhimu sana wazazi kuhimiza watoto kulala mchana kwaajili ya afya bora na ukuaji bora. Tunaweza kutoona faida yake mara moja lakini baadae tukaona matokeo  makubwa hasa kwenye ukuaji wao na uwezo wa akili zao darasani, fikra zao na mambo yanayoendana na kuepuka magonjwa kama vile ya moyo. Mhimize mtoto alale mchana kwaajili ya afya bora.

Jumatano, 5 Februari 2020

NJIA ZA KUZUIA KUTAPIKA WAKATI WA UJAUZITO



Kutapika kwa mama mjamzito inaleta kero na mama huyo kukosa raha mara nyingi. Miezi ya awali ya ujauzito hua na changamoto hii sana lakini ikiendelea inaleta karaha kabisa, unaweza kuzuia hali hii kwa njia zifuatazo.
  • Kula matunda au mkate wa kukaushwa asubui
  • kunywa vinywaji nusu saa kabla ya kula au baada ya kula. Usile na kunywa kwa wakati mmoja.
  • Kunywa maji mengi sana kuzuia upungufu wa maji mwilini (dehydration). Jitaidi kunywa lita 2.5 kila siku na pamoja na juisi ya matunda.
  • Epuka kulala baada ya chakula
  • Pata muda wa kupumzika wa kutosha na pata kusinzia mchana
  • Fanya mazoezi
  • Ndimu na tangawizi husaidia kupunguza na kuondoa kichefuchefu. Unaweza kunywa juisi ya ndimu au tikiti maji.
  • Epuka kupita sehemu yenye harufu ya chakula
  • Epuka kula vyakula vyenye pilipili au viungo vingi
  • Pata hewa (Oxygen) ya kutosha na fungua madirisha ili hewa iweze kuingia
  • Usiache kula au kuruka milo.
Hizo ni kati ya njia chache za asili kati ya nyingi. Tatizo likizidi muone daktari kwa matibabu zaidi na vipimo zaidi

Muda unaofaa kubeba mimba baada ya mimba uliyobeba kuharibika?

Ni vizuri kwanza kujua vitu vinavyoweza kusababisha mimba kuharibika.
Mimba nyingi huharibika kutokana na makosa ya ukuaji wa mtoto. Sehemu kubwa ya makosa haya huwa ni kwenye vinasaba vyake. Yanaweza kuwa ya kurithi au yasiyo ya kurithi yaliyotokea kwa bahati mbaya kwa mtoto.
Zipo pia sababu nyingine kama vile maumbile ya viuongo vya uzazi, magonjwa ya mama kama vile kisukari, magonjwa ya damu, magonjwa ya vijidudu (infection).
Pamoja na sababu za mimba kuharibika kuwa nyingi, mara nyingi linapotokea tatizo hili huwa sababu iliyosababisha haifahamiki. Hali hii husababisha akinamama wengi na wenza wao kubaki na maswali mengi kwanini imewatokea hivyo na hujiuliza kama inaweza kutokea tena kwenye ujauzito mwingine.
Mara nyingi hali hii hutokea mara moja na haijirudii. Hii ni kwa sababu makosa ya ukuaji yanayotokea bahati mbaya huwa ni jambo lenye uwezekano mdogo sana kujirudia. Hata hivyo iwapo ujauzito umeharibika kwa sababu nyingine kama vile za kimaumbile au magonjwa ya damu, uwezekano wa kujirudia huwa mkubwa iwapo hali hiyo haijagundulika na hatua stahiki kuchukuliwa.
Kujibu swali la msingi ni baada ya muda gani inafaa kubeba mimba nyingine, inategemea kama ni mara ya kwanza ujauzito kubadilika au ni hali iliyojorudia. Kama ni mara ya kwanza, unaweza kubeba ujauzito mwingine mara tuu unapopata siku zako (vizuri zaidi angalau baada ya wiki 6 baada ya ujauzito kuharibika). Kwa kipindi hiki mwili unakuwa tayari kupokea ujauzito mwingine.
Hata hivyo kwa vile swala la ujauzito kuharibika linapokelewa kwa hisia tofauti na linaowakuta, ni vizuri ukabeba ujauzito baada ya kuwa umeshakuwa katika hali ya kawaida kihisia.


Iwapo ujauzito kuharibika sio mara ya kwanza, kuna umuhimu wa kufanyiwa vipimo na daktari ili upewe ushauri juu ya kujiandaa na ujauzito mwingine. Aina ya ushauri inategemea na matokeo ya vipimo atakavyoshauri daktari. Vilevile inategemea kama ujauzito (mtoto) ulioharibika ulikutwa na tatizo lolote linalohitaji muda kulichunguza. Vipimo hivi vinaweza kuwa pamoja na vipimo vya damu, kipimo cha ultrasound na vingine.
Daktari anaweza kushauri utumie dawa za folic acid au vitamin wakati ukijiandaa na ujauzi mwingine.
Wanawake wengi (asilimia 70) waliopata tatizo la ujauzito kuharibika walifanikiwa kupata ujauzito tena na kujifungua watoto wenye afya njema. Kwahiyo usikate tamaa iwapo umekutwa na hali hii.

Njia thabiti ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU)

VVU/Ukimwi umeendelea kuwa ni moja kati ya changamoto kubwa katika sekta ya Afya duniani haswa kwa nchi zinazoendelea. Kutokana na Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), inakadiriwa kuwa, kuna watu milioni 36.9 wanaishi na virusi vya ukimwi duniani kote.
Kwa siku za karibuni, kumekuwa na matokeo chanya kwenye mapambano na ugonjwa wa ukimwi, sasa hivi watu wenye virusi vya ukimwi (VVU) wanaishi maisha yenye afya njema na kwa muda mrefu kwa msaada wa dawa za kufubaza makali ya virusi vya ukimwi (antiretroviral therapy (ART)), pia matumizi sahihi ya dawa hizi husaidia kupunguza muendeleo wa uabukizaji kwa wengine.



Kazi kubwa pia imefanyika ili kuzuia na hata kumaliza kabisa maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua.
Ingawa kuna matokeo yote hayo chanya, lakini bado kuna sehemu kubwa ya jamii bao haina uelewa juu ya ugonjwa huu, hivyo TanzMED itakuwa inakuletea dondoo chache juu ya ugonjwa huu;
1. VVU vinaweza kuambukizwa kwa njia mbalimbali kama;
  • Kuambukizwa kwa mtoto mchanga wakati akiwa tumboni, wakati wa kuzaliwa au kwa kunyonyeshwa na mama anayeishi na virusi vya ukimwi. Hivyo, kabla na baada ya kuanza kubeba ujauzito, inashauriwa kupima Afya na kuhudhuria vyema kliniki kwa ajili ya vipimo na ushauri juu na njia za kuondoa maambukizi haya.
  • Kujamiiana bila ya kinga na mtu mwenye virusi vya ukimwi
  • Kuwekewa damu yenye virusi vya ukimwi
  • Kushare vitu vyenye incha kali (sindano, viwembe, masjine za kuchorea tattoo, mikasi nk) vilivyo na virusi vya ukimwi. Watumiaji wa madawa ya kulevya wapo kwenye hatari ya kuambukizana kwakuwa wengi hutumia sindano kwa pamoja
  • Matumizi ya vifaa vya upasuaji ambavyo havijafanyiwa usafi wa kuua virusi
2. Jinsi ya kujikinga au kuzuia maambukizi ya virusi vya ukiwmi (VVU) kwa wengine
  • Hakikisha unatumia zana pindi unapofanya ngono
  • Nenda kapime na upate tiba ya magonjwa mengine ya zinaa kwani kuwa na magonjwa ya zinaa kuna uwezekano mkubwa wa kuambukizwa virusi vya ukimwi, pia kupima na kujijua mapema, kunasaiia kulinda afya yako na kuzuia kuwaambukiza wengine
  • Hakikisha damuunayowekewa imepimwa na haina virusi vya ukimwi
  • Kutahiriwa kwa wanamume kunasaidia kupunguza maambukizi 
  • Matumizi ya mapema na yaliyobora ya dawa za kufubama makali ya virusi vya ukimwi (ARV) husaidia kukufanya uishi na afya bora pia kupunguza maambukizi kwa wengine
  • Kuishi maisha yanayompendeza mungu kwa kuacha kuzini kabla na nje ya ndoa

Jumatatu, 3 Februari 2020

Msongo wa Mawazo (Sonona)

Msongo wa mawazo ni mfadhaiko wa akili anaoupata mtu kutokana na shida, taabu, dhiki, matatizo au changamoto zinazomkabili katika maisha ya kila siku. Mtu hupata msongo wa mawazo pale anaposhindwa au kukosa namna ya kukabiliana na jambo linalomsumbua.



Vitu Vinavyosababisha Mtu Kupata Msongo wa Mawazo 
Kuna sababu nyingi zinazosababisha mtu kupata msongo wa mawazo, baadhi ya sababu hizo ambazo zimegawanyika katika makundi mawili ambayo ni kibiologia na kisaikolojia.

Sababu za kibiologia 
o Mtu kurithi vinasaba kutoka kwa mzazi/ wazazi 
o Magonjwa ya muda mrefu kama UKIMWI, figo, ini, moyo nk. 

Sababu za kisaikolojia 

  • Matukio yasiyofurahisha kama Ubakaji,Uvamizi, Ajali au Kufiwa, au kutekwa nyara  
  • Majanga kama Kimbunga, Mafuriko, Tetemeko la ardhi n.k 
  • Changamoto za kila siku za maisha Ugoni, Talaka, Mimba kuharibika, Kutoa mimba, Kutengana,       Kufungwa, Kuuguza au Kukosa kazi. 
  • Matatizo sehemu za kazi Kufukuzwa kazi / Chuo, Migogoro kazini au Kustaafu kazi. 
  • Mambo ambayo yanategemewa mtu kufurahi yanaweza kumsababishia msongo wa mawazo kama     Kuoa au Kuolewa, Kuzaliwa mtoto, Kufaulu mtihani, Ajira mpya, kuhamia nyumba mpya, Kupata ujauzito nk
Dalili za Msongo wa Mawazo 
  • Maumivu ya sehemu mbalimbali za mwili hasa kichwa na kifua
  • Kuwa na huzuni na kujisikia mnyonge
  • Kusahau na kukosa uwezo wa kufikiri vyema
  • Kujihisi kuchoka na kukosa ari nya kufanya kazi, 
  • Kuwa na hofu na kutokujiamini 
  • Kushindwa kufanya maamuzi sahihi,
  • Kushindwa kula au kula sana,
  • Kukosa hamu ya tendo la ndoa
  • Kupungua uzito au kuongezeka uzito 
  • Kubadilika kwa siku za hedhi au kutokuona kabisa 
  • Kulala muda mfupi na muda mwingi kuwa macho usiku 
  • Kukosa choo kwa muda mrefu 
  • Kutaka kujiua au kuwa na mawazo ya kujiua
Athari za Msongo wa Mawazo 
Athari za Msongo wa Mawazo zinaweza kuwa za kihisia au kitabia 

Athari za Kihisia 
  • Kuwa na hofu kupita kiasi 
  • Kuwa na mfadhaiko na 
  • Kuwa na hisia za kukosa ulinzi 
  • Kusahau na kushindwa kufikiria ipasavyo 
  • Kukosa utulivu na kuwa na huzuni.
Athari Kitabia 
  • Kula sana/-kushindwa kula 
  • Kubagua aina za vyakula. 
  • Kuwa na hasira 
  • Kunywa pombe kupita kiasi au Kutumia madawa ya kulevya, 
  • Kupenda kuwa mwenyewe na kujitenga na jamii 
  • Kuwa na huzuni na kulia 
  • Kutoelewana na jamii
Namna ya kupunguza Msongo wa Mawazo 
  • Tafuta chanzo cha msongo na epuka nalo au kubaliana nalo. 
  • Kuwa na mtizamo chanya kwamba hiyo changamoto inayokukabili kwani huo sio mwisho wa maisha.
  • Fanya mazoezi ili kupunguza mzigo wa hisia unaokuelemea na huondoa msongo wa mawazo. 
  • Epuka kuwa peke yako, washirikishe watu wa karibu matatizo yako kwa kuomba ushauri 
  • Pata muda wa kutosha wa kupumzika ikiwa ni pamoja na kulala 
  • Epuka mazoea mabaya kama kunywa pombe au kutumia dawa kwa imani kwamba zitakupunguzia msongo wa mawazo 
  • Jitahidi Kula vizuri kwani mwili unategemea chakula ili uweze kufanya kazi vizuri 
  • Fanya vitu ambavyo vitakupa starehe kama kusoma vitabu, kusikiliza mziki, kwenda sehemu za burudani, na kuwa na mtu wa kukufariji.
  • Badilisha mazingira kwa kutembelea sehemu mbalimbali kama vile fukwe za bahari, mbuga za wanyama, bustani nk
  • Pata ushauri wa wataalam (daktari, mwanasaikolojia nk) 
  • Kutumia dawa kwa usahihi kila wakati na 
  • Kuhudhuria kiliniki kila wakati kama ulivyopangiwa na wataalam wa afya.